Saturday, 10 January 2015

Wafanyakazi WA RELI YA Tazara WAGOMA LEO







WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu) wameazimia kuanza mgomo leo wakidai Serikali Sh bilioni 12.5 huku wakisitisha huduma za usafiri wa treni zote za mamlaka hiyo.

Usitishwaji wa huduma hiyo unajumuisha treni zilizoko safarini kuelekea mikoani na zile ziliko njiani kurudi Dar es Salaam ambapo zitaachwa zilipofikia kabla ya vituo vinavyotakiwa kufika, ili kushinikiza mamlaka hiyo kuwalipa mishahara yao ya miezi mitano ambayo wanadai.

Maazimio hayo yalitolewa jana katika mkutano uliowakutanisha wafanyakazi zaidi ya 400, viongozi wa Trawu na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta), ulifanyika katika ukumbi wa Msimbazi Center baada ya uongozi wa mamlaka hiyo kuwazuia kukutana katika ukumbi wa Tazara.

Maazimio hayo yanaenda sambamba na siku saba zilizotolewa na Tucta kwa Tazara kuhakikisha inawalipa wafanyakazi hao mishahara yao yote, huku pia wakitaka Tucta imlete Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ili aongee na wafanyakazi hao.

Akitoa maazimio hayo, Katibu Mkuu wa Trawu Taifa, Erasto Kihwele alisema katika siku saba hizo hakuna kazi yoyote itakayoendelea hadi hapo watakapolipwa fedha zao pamoja na kusikilizwa madai yao mengine. “Tunasimamisha treni zote kwa mpigo, ile ya Makambo Kilombero, ya Dar es Salaam (Mwakyembe) na ya safari ndefu, zote zinasimama hazitafanya kazi, sababu kubwa ya kufanya hivi ni usalama wa abiria na mali zao lakini pia kuepusha hasara ya mamilioni yaliyotumika kununulia mabehewa,” alisema Kihwele.

Alisema wanahitaji kuonana na Waziri Mwakyembe kutokana na awali walimweleza malalamiko yao lakini hayakufanyiwa kazi, hivyo wanahitaji kuonana naye tena ili kujadili hatma ya Tazara pamoja na kuwataja viongozi wanaotaka aondoke nao.

Kwa upande wake, Rais wa Tucta, Gratian Mukoba alisema, shirikisho hilo linaungana na wafanyakazi hao katika kusitisha shughuli za utoaji huduma, huku akisema uamuzi huo utafanya siku saba walizotoa ziwe ni za kweli kwa wao kupata haki yao.

Akizungumzia kuhusu maombi ya wafanyakazi hao kutaka kufikisha salamu zao kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mwakyembe, Mukoba alisema, haoni sababu ya kumweleza Rais malalamiko hayo kutokana na kuwa ni ngazi ya mwisho ambayo wanatakiwa kwenda baada ya ngazi zote kushindwa.
“Siwezi kwenda kuzungumza na Rais kwa sababu yeye ndiyo mwenye maamuzi ya mwisho, ni kama rufaa na hata Mwakyembe siwezi kuzungumza naye, nitamleta mbele yenu muongee naye wenyewe,” alisema Mukoba huku akishangiliwa na wafanyakazi hao.

Alisema mamlaka hiyo kwa sasa kila kukicha inaitamani jana kutokana na kuandamwa na matatizo mbalimbali ikiwamo madai ya wafanyakazi na shirika hilo kushindwa kujiendesha kibiashara, “Ukiona leo inaitamani jana ujue kuna tatizo, kwa kawaida jana ndiyo inatakiwa kuitamani leo, lakini kwa Tazara ni kinyume kuna matatizo,” alisema.

Awali akisoma risala ya wafanyakazi wa Tazara, Naibu Katibu Mkuu wa Trawu (Taifa), Patrick Nyaseche alisema wafanyakazi hao wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kutolipwa mishahara yao kwa wakati, hivyo kuishi kama ombaomba.

Alisema kipindi chote wafanyakazi hao walichokuwa wakiendelea bila malipo walikuwa wakifanya kwa uzalendo wao na si vinginevyo, huku akisema sheria zilizopitwa na wakati zinachangia kuharibu mamlaka hiyo.
“Ukiangalia unakuta gharama za usafirishaji wa mizigo ziko juu sana, mtu unalipa Dola za Marekani 50 (Sh 75,000) kusafirishwa mzigo wako hauletewi mpaka dukani, lakini unalipa pesa hiyo hiyo kusafirisha kwa lori linalokuletea mpaka mlangoni kwako, hii inasababishwa na hawa mameneja ambao hatuwataki,” alisema Nyaseche.

Mmoja wa wafanyakazi waliopata fursa ya kuchangia katika mkutano huo, Teresia Magatila alisema, kutokana na usalama wa afya zao na mali za mamlaka hiyo hawako tayari kuendesha huduma yoyote, huku akishutumu kuwa viongozi wa juu wa mamlaka hiyo wanaihujumu.
“Kuna kiongozi mmoja alisema mtaimba solidarity (mshikamano) mpaka mikono ichomoke lakini kwenye hii nafasi sitoki, viongozi wa aina hii ndiyo wametufikisha hapa,” alisema.

Mamlaka hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto pamoja na migogoro ya mara kwa mara na wafanyakazi wake kwa kutowalipa wafanyakazi wake mishahara jambo linalochangia kuyumba kwa mamlaka hiyo.

No comments:

Post a Comment